Nafunga macho na kuiona Tanzania Yangu,
Nawaona wanawake wakitembea mwendo mrefu,
Wana angua vicheko lakini ndani wana uchungu
Wanafarijiana kwa kua na uchangamfu.
Kwa nusu siku wametembea kilometa kumi juani
Wakitafuta angalau ndoo ya maji kisimani
Wamesikia habari za maendeleo redioni
Lakini hawazioni kijijini.
Tanzania Oye! Ni mvumo wa baragumu za Siasa
Maliasili ni urithi wetu sote, lakini wachache wanufaika
Wenye mapenzi ya dhati na Tanzania amka SASA
Angaza penzi lako Tanzania ipate komboka
Wametudanganya! Wamesema sisi ni masikini na tumewaamini
Hatukujua kua umasikini ni namna ya kufikiri
Angalia ardhi ilivyo na utajiri
Imejaa rotuba na imeshiba madini
Muziki wetu una mdundo mpya
“Msiulize maswali”, “Jikazeni”, ni mdundo wa zamani
Usiogope kuuliza “ziko wapi Zahanati za Afya?”
Thubutu kuchangia mawazo yako kudumisha amani
Elimu ni chanzo cha maendeleo yetu
Sio kufaulu vizuri darasani ila kuishi ulichofuzu
Wengi wametoka kwetu lakini hawakua wa kwetu
Wamesahau ya nyumbani, wamekua mazuzu
Tanzania Yangu ni nchi ya maziwa na asali
Inuka mtanzania, pamoja tutafika mbali
Hakuna lisilowezekana kwao waaminio
Futa mavumbi, kanza msuli, tupige mbio
Ninaipenda Tanzania Yangu!

No comments:
Post a Comment